
Taarifa za
kiutafiti zinautaja mti huo kwa jina la Mvunge, ukiwa na uwezo wa kukuza
makalio, matiti na kurefusha uume.
Kaimu
Msajili wa Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini, Dk Naomi Mpemba anasema kuwa mmea
huo ambao huwa ni mti mkubwa upo na kwamba una uwezo mkubwa wa kukuza maumbile
hayo.
Anabainisha
kuwa mmea huo ambao hukua na kuwa mti mkubwa huzaa matunda yanayotumika kama
dawa na unapatikana wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga, Pwani, Mbeya, Morogoro na
baadhi ya mikoa nchini.
“Tulifuatilia
na kutambua kuwa mti huo upo maeneo hayo na unatumiwa zaidi na waganga, hata
picha za mti huo tunazo,” anasema Dk Mpemba na kuongeza:
“Jina jingine unaitwa Miegeya, mara nyingi
unastawi katika maeneo yenye ardhi ya unyevunyevu, una tabia ya kustawi kama
Mwembe na matunda yake huonekana kufanana na Mbuyu.”
Hata hivyo,
anasema kuwa asilimia kubwa ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala wanaotumia
dawa hiyo ni wale wasiokuwa na usajili kutoka baraza hilo, hivyo kufanya huduma
hizo kinyume cha utaratibu.
“Kwa mujibu wa masharti yaliyopo katika agizo la Serikali kwa waganga hao, miiko, maadili
na utendaji wa kazi zao umeelekeza kuwepo na usiri na kuaminiwa, kwa hiyo sisi
tunaamini wanaojitangaza kutibu mambo hayo ni matapeli,” anasema Dk Mpemba.
Huku
akionyesha wasiwasi wa kutoa picha za mti huo, Dk Mpemba alisema kwamba endapo
utaonekana wazi kupitia vyombo vya habari, jamii inaweza kuathirika kwa sehemu
kubwa kuutafuta.
Dk Mpemba
alitahadharisha kuwa matumizi ya mmea huo siyo mazuri kwa vijana, badala yake
akasisitiza matumizi ya lishe bora kupitia vyakula vinavyojenga mwili.
“Suluhisho
ni lishe na siyo kuhangaika na dawa za ajabu, tatizo lenu vijana vyakula ni
chipsi, mayai, nguvu zikiwaishia matokeo yake ndiyo mnaanza kutafuta dawa za
kurefusha sehemu za siri, haitawasaidia, dawa ni lishe tu,” alisisitiza Dk
Mpemba.
Mkuu wa
Kitengo cha Utafiti wa Tiba za Asili wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba nchini NIMR,
Dk Hamis Malebo, alisema Nimr inaufahamu mmea huo, ingawa haijaufanyia utafiti
wa kuthibitisha uwezo wake huo.
Alisema mmea
huo kisayansi unaitwa Kigelia Africana na unapatikana katika maeneo mengi ya
Afrika.
“Masuala ya
tiba asilia yanaweza wakati mwingine kuwa na utata na sisi hatuwezi kusema sana
kwa sababu hatujafanya utafiti,” alisema Dk Malebo.
Alisema Nimr
haiwezi kuzungumza kwa undani kwa sababu bado haijawathibitisha watu waliowahi
kupata tiba ya mmea huo, wala haijahakiki chochote kuhusu matunda au mizizi ya
mti huo kufanya kazi.
Mbali na
kukithiri kwa matibabu ya dawa hizo, Serikali imeendelea kutoa onyo kali kwa
waganga wote wanaotoa huduma bila kusajiliwa kama ilivyoagizwa.
Matumizi
mengine ya Mvunge
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa mti huo umekuwa ukitumika kwa miaka
mingi, ambapo baadhi ya wazazi ama vijana binafsi huamua kwenda kwa wataalamu
wa tiba za asili na kupatiwa huduma hiyo baada ya kubainika kuwa maumbile yao
kuwa madogo isivyo kawaida.
Mti huo pia
unaelezwa kutumika kuponya wazee ambao viungo vyao vimepoteza uhalisia wake
pamoja na kutibu ugonjwa wa kuziba njia ya haja ndogo, ukipata umaarufu katika
maeneo ya Wilaya za Handeni, Kilindi na Bagamoyo mkoani Pwani,ambapo hupatikana
zaidi maeneo ya mabondeni.
Mizizi,
matunda, mbegu za matunda, magamba ya mti na majani vyote hutumika kama dawa na
chakula.
Matunda
yaliyoiva na mabichi ya mti huo ni sumu kwa binadamu, lakini baadhi ya watu
hukausha matunda hayo na kuyachanganya katika pombe za kienyeji ili kuongeza
ladha.
Karibu kila
sehemu ya mti huu hutumika kama dawa ya asili, kwa mfano kulainisha chakula,
kutibu kushindwa kupumua, kutibu majeraha na maradhi ya ngozi.
Utafiti wa
mti huo katika kutibu bakteria, fungasi na uvimbe unaendelea kufanyika katika
nchi za Korea, Japan na India.
JE VIPI KUHUSU USHUHUDA
HUU:
Mmoja wa
watu wanaotoa tiba hiyo ya asili wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, akifahamika
kwa jina la Dk Ramadhani Chenyewe, anasema kuwa ametibu watu wengi wakiwamo
vijana na wazee kutoka ndani na nje ya wilaya hiyo, waliohitaji kuimarishwa
nyeti zao.
Chenyewe
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Jadi (MACO) wilayani Handeni,
anafafanua kwamba, kwa kutumia dawa hiyo msimu wa mvua nyingi, nyeti hukua kwa
haraka katika muda usiozidi mwezi mmoja, kutokana na tunda la mti huo kukua
haraka.
“Hilo jambo
ni la kweli wengi ninaowatibu wana tatizo uume ni mdogo, na wengine nao ni
wazee ambao wanaona mabadiliko katika sehemu hizo kwa kuwa ndogo, tofauti na
awali. Basi wakija huwa ninaangalia kwanza kama kweli ni ndogo, baada ya
kuthibitisha ndipo ninamuongezea,” anasema Dk Chenyewe.
Aliongeza: “Nimewasaidia wengi, tiba yenyewe ni
kwamba unakwenda kwenye mti kabla ya kufanya chochote, unaufanyia kitu kama
tambiko, baada ya hapo ndipo shughuli ya tiba zinaanza kwa kutumia pia matunda
ya mti huo ambayo yanakua kwa urefu.”
Hata hivyo,
anaonya kuwa kazi hiyo inahitaji uangalizi mkubwa kwa vile inaweza kuwa kubwa
kupita kiasi, hali inayoweza kusababisha madhara kwa mwenza.
Amewataka
wanajamii kuacha kwenda kwa waganga kukuza nyeti zao kwa nia ya tamaa ya kutaka
kuwakomoa wenzi wao, akisema hilo siyo kusudio la kuanzishwa kwa tiba hiyo ya
aina yake.
Mmoja wa
watu waliopatiwa tiba hiyo ya kukuza nyeti, ambaye ni mkazi wa mjini Handeni,
aliyeomba jina lake lisitajwe, anasema kwamba alikwenda kwa waganga hao kutokana
na kuona kiungo chake hakilingani na vya wenzake.
“Mimi wakati
tunacheza na wenzangu hasa kwenda kuogelea, nilikuwa nashangaa mbona ya kwangu
ni ndogo sana ukilinganisha na wenzangu. Nikamweleza babu yangu, ambaye naye
aliniangalia kisha akanishauri twende kwa mganga ambaye anakuza kwa kutumia
yale Mavungwe,” anasema kijana huyo mwenye umri wa miaka 27.
Kijana huyo
anadai kwamba alitibiwa na kufikia malengo yake kwa muda wa mwezi mmoja, tangu
kufanyiwa tiba katika mti huo maarufu sana kwa waganga wa jadi mkoani Tanga.
0 comments :
Post a Comment